29 May
Kuonekana kwa Mungu Kumeleta Enzi Mpya

Kuonekana kwa Mungu Kumeleta Enzi Mpya

    

Mpango wa Mungu wa miaka elfu sita ya usimamizi unaisha, na lango la ufalme limefunguliwa kwa wale ambao wanatafuta kuonekana kwa Mungu. Ndugu wapendwa, mnasubiri nini? Mnatafuta nini? Mnasubiri kuonekana kwa Mungu? Mnazitafuta nyayo za Mungu? Kuonekana kwa Mungu kunatamaniwa sana! Ni vigumu, kiasi gani kupata nyayo za Mungu! Katika enzi kama hii, katika dunia kama hii, lazima tufanye nini ili tushuhudie kuonekana kwa Mungu? Sharti tufanye nini ili tufuate nyayo za Mungu? Wale wote wanaosubiri kuonekana kwa Mungu wanakumbana na maswali kama haya. Nyinyi nyote mmewahi kuyafikiria zaidi ya mara moja—ila matokeo ni gani? Mungu hujidhihirisha wapi? Nyayo za Mungu zipo wapi? Mmepata majibu? Majibu ya watu wengi yangekuwa: Mungu hudhihirika miongoni mwa wale wanaomfuata na nyayo Zake zimo miongoni mwetu; ni rahisi hivyo! Mtu yeyote anaweza kutoa jibu kwa kutumia mbinu fulani, lakini je, mnafahamu kuonekana kwa Mungu ni nini, na nyayo za Mungu ni nini? Kuonekana kwa Mungu hurejelea kuwasili Kwake duniani kufanya kazi Yake. Akiwa na utambulisho na tabia Yake, na katika mbinu Yake ya asili, Yeye hushuka miongoni mwa wanadamu kufanya kazi ya kuanzisha enzi mpya na kukamilisha enzi nyingine. Kuonekana kwa aina hii si aina fulani ya sherehe. Si ishara, picha, muujiza, au ono kuu, na hata zaidi si mchakato fulani wa kidini. Ni ukweli halisi ambao waweza kushikwa na kuonekana. Kuonekana kama huku si kwa ajili ya kufuata taratibu, au kwa ajili ya shughuli ya muda mfupi; ni, badala yake, kwa ajili ya hatua ya kazi ya mpango Wake wa usimamizi. Kuonekana kwa Mungu daima ni kwenye maana na daima huenda pamoja na mpango wa usimamizi. Kuonekana huku ni tofauti kabisa na udhihirisho wa uongozi wa Mungu, utawala na kupata nuru kwa mwanadamu. Mungu hufanya kazi kubwa kila mara Anapojifunua. Kazi hii ni tofauti na enzi yoyote nyingine. Haiwezi kufikirika na mwanadamu na haijawahi kupitiwa mwanadamu. Ni kazi ambayo huanzisha enzi mpya na kutamatisha enzi ya awali, na ni aina mpya ya kazi na iliyoboreshwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu; aidha, ni kazi ya kuleta wanadamu katika enzi mpya. Huo ndio umuhimu wa kuonekana kwa Mungu.

Katika wakati uo huo wa kuelewa kuonekana kwa Mungu, mnapaswa kutafuta nyayo za Mungu vipi? Swali hili si gumu kueleza: Palipo na kuonekana kwa Mungu; mtapata nyayo za Mungu. Maelezo kama haya yanaonekana yapo wazi, ila si rahisi kuelezea kwani watu wengi hawafahamu pale Mungu anapojidhihirisha, wala pale ambapo Angependa kujidhihirishia ama iwapo Anapaswa kujidhihirisha. Wengine kwa msukumo huamini kuwa palipo na kazi ya Roho Mtakatifu kuna kuonekana kwa Mungu. Ama sivyo watu huamini kuwa palipo na watu mashuhuri wa kiroho ndipo Mungu huonekana. Vinginevyo, wanaamini kuwa palipo na watu wanaojulikana vyema ndipo Mungu huonekana. Kwa sasa tusishauriane ikiwa imani hizi ni sahihi au la. Kujibu swali kama hilo, kwanza ni lazima tuwe wazi kuhusu lengo: tunazitafuta nyayo za Mungu. Hatutafuti viongozi wa kiroho, wala kutafuta watu mashuhuri; tunafuata nyayo za Mungu. Kwa hivyo, kwa kuwa tunatafuta nyayo za Mungu, ni sharti tufuate mapenzi ya Mungu, maneno ya Mungu, matamshi ya Mungu—kwani palipo na maneno mapya ya Mungu, kuna sauti ya Mungu, na palipo na nyayo za Mungu, pana matendo ya Mungu. Palipo na maonyesho ya Mungu pana kuonekana kwa Mungu, na palipo na kuonekana kwa Mungu, pana ukweli, njia na uzima. Mlipokuwa ukitafuta nyayo za Mungu, mliyapuuza maneno haya kuwa “Mungu ndiye ukweli, njia na uzima.” Kwa hivyo, watu wengi wanapoupokea ukweli, hawaamini kuwa wamepata nyayo za Mungu na hata zaidi hawasadiki kuonekana kwa Mungu. Kosa hilo ni kuu kiasi gani! Kuonekana kwa Mungu hakuwezi kulinganishwa na fikira za mwanadamu, sembuse Mungu kuonekana kwa amri ya mwanadamu. Mungu hufanya uamuzi Wake mwenyewe na huwa na mipango Yake Afanyapo kazi; aidha, Ana malengo Yake, na mbinu Zake. Si lazima Ajadiliane kazi Azifanyazo na mwanadamu au Atafute ushauri wa mwanadamu, sembuse kumfahamisha kila mtu kuhusu kazi Yake. Hii ndiyo tabia ya Mungu na, zaidi ya hayo, inafaa kutambuliwa na kila mmoja. Kama mnatamani kushuhudia kuonekana kwa Mungu, kama mnatamani kufuata nyayo za Mungu, basi kwanza ni sharti mzishinde dhana zenu. Ni sharti muache kudai kuwa Mungu afanye hiki au kile sembuse kumweka Yeye ndani ya mipaka yenu wenyewe na kumwekea upeo kwa dhana zenu. Badala yake, mnafaa kujua ni vipi mtazitafuta nyayo za Mungu, na vipi mnapaswa kukubali kuonekana kwa Mungu na ni vipi mnapaswa kutii kazi mpya ya Mungu; hiki ndicho kinapaswa kufanywa na mwanadamu. Kwa kuwa mwanadamu si ukweli, na hamiliki ukweli, mwanadamu anafaa kutafuta, kukubali na kutii.

Bila kujali kama wewe ni Mmarekani, Mwingereza, au mtu wa taifa jingine, ni lazima utoke nje ya mipaka yako, ni lazima ujipite, na ni sharti uione kazi ya Mungu kama kiumbe wa Mungu. Kwa njia hii, hutaweka vikwazo katika nyayo za Mungu. Kwa sababu, leo, watu hufikiri kuwa haiwezekani Mungu kudhihirika katika nchi au taifa fulani. Umuhimu wa kazi ya Mungu una undani kiasi gani, na kuonekana kwa Mungu kuna maana ilioje! Vinawezaje kupimwa kwa dhana na fikira za mwanadamu? Na ndiyo maana Ninasema kuwa unafaa kujiondoa katika dhana za uraia wako au kabila lako unapokutafuta kuonekana kwa Mungu. Kwa njia hii, hutafungwa na dhana zako mwenyewe; kwa njia hii, utahitimu kukaribisha kuonekana kwa Mungu. Vinginevyo, daima utakuwa gizani na hutapata kibali cha Mungu.

Mungu ni Mungu wa wanadamu wote. Hawi mali binafsi ya nchi au taifa lolote na hufanya kazi ya mpango Wake bila kuzuiwa na mfumo wowote, nchi au taifa. Labda hujawahi kuwazia mfumo huu, au labda wewe hukana kuwepo kwake, au labda nchi au taifa ambapo Mungu huonekana limebaguliwa na lina maendeleo duni sana duniani. Na bado Mungu ana busara Yake. Na uwezo Wake kupitia ukweli na tabia Zake kwa hakika Amepata kundi la watu wenye mawazo sawa na Yeye. Na Amepata kundi la watu ambao alitaka kutengeneza: kundi lililoshindwa Naye, watu ambao wameyavumilia majaribu machungu na aina zote za mateso na wanaweza kumfuata mpaka mwisho. Malengo ya kuonekana kwa Mungu, bila vizuizi vya nchi yoyote, ni kumruhusu Akamilishe kazi ya mpango Wake. Kwa mfano, Mungu alipopata mwili kule Uyahudi, lengo Lake lilikuwa kutimiza kazi ya msalaba na kuwakomboa wanadamu wote. Na bado Wayahudi waliamini kuwa Mungu asingeweza kulifanya hili, na wakafikiri kuwa Mungu asingeweza kuwa mwili na kuchukua umbo la Bwana Yesu. “Kutowezekana” kwao kukawa msingi wa kumshutumu na kumpinga Mungu na hatimaye ikawa kuangamizwa kwa Israeli. Leo hii, watu wengi wamefanya kosa lile lile. Wanatangaza kuonekana kwa Mungu ambako kumekaribia, na vilevile kukushutumu kuonekana huku; “kutowezekana” kwao kwa mara nyingine kunabana kuonekana kwa Mungu katika mipaka ya dhana zao. Na kwa hivyo Nimeona watu wengi wakicheka na kuanguka baada ya kuyasikia maneno ya Mungu. Kicheko hiki kinatofautianaje na shutuma na kukufuru kwa Wayahudi? Hamna moyo wa dhati katika kukabiliana na ukweli, sembuse kutamani ukweli. Nyinyi huchunguza tu kama vipofu na kusubiri kwa utepetevu. Mtajifaidi na nini kwa kutafiti na kusubiri kwa njia hii? Je, mnaweza kupata uongozi binafsi wa Mungu? Kama huwezi kuyang’amua matamshi ya Mungu, umehitimu vipi kushuhudia kuonekana kwa Mungu? Mahali ambapo Mungu anajitokeza, kuna maonyesho ya kweli, na kuna sauti ya Mungu. Ni wale tu wanaoukubali ukweli ndio watakaoisikia sauti ya Mungu, na ni hao tu waliowezeshwa kushuhudia kuonekana kwa Mungu. Weka dhana zako kando. Tafakari na kusoma maneno haya kwa makini. Ukitamani ukweli, Mungu atakupa nuru ya kuyafahamu mapenzi Yake na maneno Yake. Wekeni kando mitazamo yenu ya “haiwezekani”! Kadiri watu wanavyozidi kuamini kuwa jambo fulani haliwezekani, ndivyo uwezekano wa utukiaji wake unavyoendelea kujiri, kwani ufahamu wa Mungu hupaa juu kuliko mbingu, mawazo ya Mungu yako juu ya yale ya mwanadamu, na kazi ya Mungu inapita mipaka ya fikira za mwanadamu. Kadiri kitu kinavyokuwa hakiwezekani, ndivyo kunavyokuwepo na ukweli wa kutafutwa; kadiri kitu kilivyo nje ya mipaka ya dhana na fikira za mwanaadamu, ndivyo kinavyozidi kuwa na mapenzi ya Mungu. Kwani bila kujali Mungu anajidhihirishia wapi, Mungu bado ni Mungu, na kiini chake hakitawahi kubadilika kwa sababu ya mahali ama namna ya kuonekana Kwake. Tabia ya Mungu hubaki kuwa vilevile bila kujali nyayo Zake ziko wapi. Bila kujali nyayo za Mungu zilipo, Yeye ndiye Mungu wa wanadamu wote. Kwa mfano, Bwana Yesu si Mungu tu wa Waisraeli, lakini vilevile ni Mungu wa watu wote wa Asia, Ulaya, na Marekani, na hata zaidi, ndiye Mungu pekee wa ulimwengu mzima. Hivyo basi, tuyatafute mapenzi ya Mungu na tugundue kuonekana Kwake kutoka kwa matamshi Yake na tufuate nyayo Zake. Mungu ndiye ukweli, njia na uzima. Maneno Yake na kuonekana Kwake yanakuwepo sawia, na tabia na nyayo Zake daima zitapatikana na wanadamu. Ndugu wapendwa, natumaini kwamba mnaweza kuona kuonekana kwa Mungu katika maneno haya, na kwamba mtaanza kuzifuata nyayo Zake kuelekea enzi mpya, na hadi katika mbingu mpya yenye kupendeza na dunia mpya iliyoandaliwa kwa wale wanaosubiri kuonekana kwa Mungu.

Chanzo: Kuonekana kwa Mungu Kumeleta Enzi Mpya


Maoni
* Barua pepe haitachapishwa kwenye wavuti.
I BUILT MY SITE FOR FREE USING